CHADEMA yaahirisha "Oparesheni UKUTA"
WEDNESDAY , 31ST AUG , 2016
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuahirisha mikutano na maandamano yake (UKUTA) ili kutoa nafasi kwa viongozi wa dini, serikali, vyombo vya dola na wadau kujadiliana kufikia muafaka.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ametangaza rasmi , kusitisha maandamano na mikutano ya siasa iliyokuwa ifanyike nchi nzima kuanzia kesho Septemba Mosi ili , kupisha nafasi ya viongozi wa dini kukutana na Rais Dkt. John Magufuli kutafuta suluhu ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Mbowe amesema CHADEMA imefikia uamuzi huo muhimu baada ya vikao na wito kutoka kwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja na asasi za kiraia.
“Viongozi wa dini na asasi za kiraia wametuomba, tusitishe maandamano hayo ili wapate nafasi ya wiki tatu mwezi huu kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ili kutafuta suluhu ya kisiasa na kama ikishindikana Oktoba Mosi maandamano hayo yataratibiwa upya” amesema Mbowe
Mbowe amesema sababu nyingine ni kuwasubiri wenzao kutoka chama cha wananchi CUF, ambao bado wanakabiliwa na michakato ya uchaguzi ndani ya chama chao, ili waungane na kuwa nguvu moja.
Amelaani vitendo vya kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, ambapo amesema hadi leo, inakadiriwa wanachama na viongozi wa CHADEMA zaidi ya 230 wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi.
Aidha Mbowe amewataka wana Chadema na wafuasi wa chama hicho kuwa watulivu wakati wakisubiri viongozi wa dini kufanya mazungumzo hayo ili haki yao ya kikatiba iweze kupatikana.
No comments:
Post a Comment