KESHA LA ASUBUHI
Jumatatu, Machi 6
Njia Tofauti
_Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia_. *Yohana 3:36*.
Yakobo na Esau walikutana kando ya kitanda cha baba yao alipokuwa katika hatua ya kufa. Wakati fulani kaka mkubwa alikuwa akitazamia muda huu kama fursa ya kulipiza kisasi, lakini hisia zake zilibadilika kabisa baadaye. Yakobo pia, akiwa ameridhishwa kabisa na baraka za kiroho za uzaliwa wa kwanza, aliachia urithi wote wa mali ya baba yake kwa kaka yake – huu ukiwa urithi pekee ambao Esau aliutafuta au kuuthamini…
Wote wawili; Esau na Yakobo walikuwa wameelekezwa katika kumjua Mungu na wote walikuwa huru kutembea katika amri zake na kupokea fadhila zake; lakini sio wote waliochagua kufanya hilo. Hawa ndugu wawili walichagua kwenda njia tofauti na njia zao zingeendelea kugawanyika zaidi na zaidi.
Kwa Esau kufungiwa nje ya baraka za wokovu haikuwa suala la uchaguzi holela kwa upande wa Mungu. Karama za neema yake kupitia kwa Kristo ziko huru kwa wote. Hakuna uchaguzi isipokuwa ule ambao mtu mwenyewe huufanya ambao kwa huo mtu anaweza kuangamia… Kila nafsi huchaguliwa ambayo itatimiza wokovu wake yenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Anakuwa amechaguliwa yeye atakayevaa silaha na kupigana vita vizuri vya imani. Anakuwa amechaguliwa yeye atakayekesha katika sala, atakayeyachunguza Maandiko na kuyakimbia majaribu. Anakuwa amechaguliwa yeye atakayedumu katika imani na yeye atakayekuwa mtiifu katika kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Utoaji wa ukombozi uko huru kwa wote; matokeo ya ukombozi yatafurahiwa na wale watakaokuwa wametekeleza masharti.
Esau alikuwa amedharau baraka za agano. Alithamini ile ya kidunia kuliko uzuri wa kiroho na akapokea kile alichotamani. Kutokana na uchaguzi wake mwenyewe ndiyo maana alitenganishwa na watu wa Mungu. Yakobo alichagua urithi wa imani. Alijaribu kuupata kwa ujanja, hila na udanganyifu; lakini Mungu aliruhusu dhambi yake ili ipate kusahihishwa… Chembechembe ovu za tabia ziliteketezwa kwenye tanuru la moto, dhahabu ya kweli ikasafishwa, hadi imani ya Ibrahimu na Isaka ilipoonekana iking’aa ndani ya Yakobo.
No comments:
Post a Comment