CHUO CHA MIPANGO- DODOMA CHAHIMIZA MATUMIZI YA TAFITI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI
Na Benny Mwaipaja,WFM
Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini na katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”. Alifafanua Prof. Lokina
Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama Chololo Ecovillage unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma, ambao huwafundisha wanakijiji njia bora za uzalishaji mali, hivyo kuwafanya baadhi ya Wananchi waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza kupata mazao ya kutosha na kuongeza pato lao.
Wajumbe wa mkutano wa Mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake kiuchumi hapa nchini uliokishirikisha Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini –Dodoma na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), wakiingia kwenye ukumbi wa Mikutano mmoja Jijini Dar es salaam, siku ya kwanza ya mkutano huo wa Siku mbili.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano uliohusu changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi wakati wa mkutano uliowashirikisha wadau wa maendeleo kutoka ndani nan je ya nchi na kuandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini-Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo akichangia mada mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoathiri uchumi wa wananchi vijijini nchini Tanzania, zilizowasilishwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini-Dodoma, na kufanyika Jijini Dar es salaam.
BONYEZA HAPA KUPATA APP YA 4SN NEWS
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.sn.news&hl=en
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment