Yanga vs Azam ndio game inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka usiku wa leo kuanzia majira ya saa 2:15 usiku ikiwa ni mchezo wa kukamilisha mechi za Kundi B katika michuano ya Mapinduzi Cup 2017.
Mechi hii itakuwa ni ya kuvutia kwa sababu ya upinzani wa timu hizi uliopo kuanzia kwenye ligi kuu Tanzania bara, lakini kwenye michuano hii ya Mapinduzi timu hizi zinakutana kwenye hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo.
Michuano ya mwaka uliopita, timu hizi zilikuwa kwenye kundi moja, mechi yao ilimalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1. Azam walianza kufunga goli lao kupitia kwa Kipre Tchetche (kwa sasa hayupo tena Azam) lakini Bosou alisawazisha dakika za lala salama.
Yanga inaongoza kundi lake (Kundi B) ikiwa na ponti sita baada ya kushinda mechi zake za mbili za kwanza (Jamhuri 0-6 Yanga na Yanga 2-0 Zimamoto). Wakati Azam wao wanashikilia nafasi ya pili kwa pointi zao nne baada ya kushinda mechi moja (Zimamoto 0-1 Azam) lakini mchezo wao wa pili wakatoka suluhu (Azam0-0 Jamhuri).
Jamhuri ina pointi moja hadi sasa baada ya kupata suluhu dhidi ya Azam huku Zimamoto yenyewe ikiwa bila pointi baada ya kupoteza mechi zake mbili ilizofungwa na Yanga na Azam.
Yanga ndio timu pekee iliyoweza kufunga magoli mengi kwenye michuano ya msimu huu huku safu yake ya ulinzi ikiwa imara, Yanga imefunga jumla ya magoli nane katika mechi mbili yenyewe ikiwa haijaruhusu bao.
Azam wana goli moja tu ambalo lilifungwa na Shabani Idd kwenye mechi yao dhidi ya Zimamoto lakini safu yao ya ulinzi haijaruhusu bao.
Kwa upande wa Yanga yenyewe tayari imefuzu kucheza hatua ya nusu fainali huku Azam ikiwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele ukilinganisha na Jamhuri yenye pointi moja. Hata kama Azam ikifungwa na Yanga halafu Jamhuri ikashinda mechi yake ya leo jioni timu hizo zitalingana pointi lakini Azam itakuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa tofauti ya magoli.
Azam vs Yanga ni vita ya kusaka heshima, kocha wa Yanga George Lwandamina hatopenda kupoteza mechi hiyo licha ya timu yake kufuzu hatua ya nusu fainali sawa na kocha wa muda wa Azam Idd Cheche ambaye timu yake haikucheza soka la kuvutia ilipokutana na Jamhuri kwenye mechi iliyopita.
Msuva amekuwa tishio kwenye michuano hii akiwa ameshafunga magoli manne (magoli mawili kila mechi) na kusaidia kupatikana kwa magoli mengine. Kwa sasa yupo kwenye kiwango bora sana na anaweza kufanya chochote dakika yoyote.
Katika mahojiano yangu na Msuva baada ya mchezo uliopita dhidi ya Zimamoto ambapo alifunga magoli yote mawili na kukosa mkwaju wa penati, alisema malengo yake ni kuibuka kinara wa mabao na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano.
Ukiachana na Msuva, Ngoma tayari pia amesha weka kambani magoli mawili aliyoyafungwa kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Jamhuri. Kamusoko ana goli moja na Juma Mahadh pia ana goli moja, hii inamaanisha unapocheza na Yanga inabidi kuwa makini kwa sababu mchezaji yeyote anaweza kufunga bao.
Kwa Msuva huyu, Azam itatoka?
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment