Na Baraka Mbolembole
 Mshambulizi  Juma Ndanda Liuzio aliye Simba SC kwa mkopo akitokea  Zesco United ya Zambia anaamini mechi ya Jumatano hii vs Mtibwa Sugar  itakuwangumu kwa kila upande hasa akichukulia ugumu wa kikosi hicho cha  Turiani kinapocheza katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya timu  kubwa nchini (Simba na Yanga SC).
 Liuzio alicheza kwa misimu mitatu Mtibwa kabla ya kuuzwa Zesco United  miaka miwili na nusu iliyopita ataikabili timu yake hiyo ya zamani  ambayo ilimlea na kumkuza kimpira kwa mara ya kwanza katika mchezo wa  ligi kuu Tanzania Bara.
 “Mechi yetu dhidi ya Mtibwa itakuwa ngumu sana kwa sababu Mtibwa huwa  wagumu sana wanapokuwa nyumbani. Upande wangu nimejiandaa vizuri  kimwili na kiakili. Sina presha yoyote na nitapambana kuisaidia timu  yangu kupata ushindi,” anasema Liuzio nilipofanyanae mahojiano Jumatatu  hii.
 Wachezaji wengi wa kulipwa husita kushangilia pindi wanapofunga dhidi  ya timu zao za zamani-hasa zile zilizowasaidia kufika walipo,  nilimuuliza Liuzio kama atashangilia ikitokea akafunga katika mchezowa  Jumatano hii.
 “Kwa kweli sitashangilia nikifunga katika mchezo dhidi ya Mtibwa.  Nitafanya hivyo kutokana na kuiheshimu timu hiyo iliyogundua kipaji  changu na kukiendeleza. Walinitunza vizuri na hadi kufika hapa nilipo ni  kwa sababu nilipitia Mtibwa. Nawaheshimu sana.”
 Liuzio alicheza michezo sita ya Simba katika michuano ya Mapinduzi Cup 2017 na kufunga goli moja.
 “Michuano ya Mapinduzi imenisaidia sana, kwanza nimefahamu Simba  wanavyocheza pia wachezaji wenzangu tayari nimewafahamu vizuri. Niko  tayari kucheza katika mfumo wowote na napenda kuwaambia mashabiki wa  Simba wajitokeze kwa wingi siku ya mchezo kutusapoti kadri ya uwezo wao  na sisi tutajituma kwa uwezo wetu kuhakikisha tunapata ushindi.”
Juma Liuzio: ‘Sitashangilia nikiifunga Mtibwa Jumatano, ni mechi ngumu ila tutashinda…’
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
 


No comments:
Post a Comment