Na Baraka Mbolembole
 Kiungo-mshambulizi wa Mtibwa Sugar, Vicent Barnabas ametamba  hawatishiki na kiwango cha Simba SC msimu huu.  Timu hizo mbili  zinakutana siku ya Jumatano hii zikiwa katika nafasi tofauti katika  msimamo wa ligi kuu.
 Simba wanaongoza wakiwa na alama 44 baada ya kucheza michezo 18 na  Mtibwa wapo nafasi ya nne wakiwa na pointi 30 baada ya kushuka dimbani  mara 18 pia.
 Katika miaka sita ya hivi karibuni, Mtibwa imepoteza mchezo mmoja tu  dhidi ya Simba katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro-walifungwa 1-0 msimu  uliopita  huku wakipoteza michezo miwili mfululizo ya ligi dhidi ya  wababe hao wa zamani katika soka la Bara. Walifungwa 2-0 katika mchezo  wa kwanza msimu huu na 1-0 katika mchezo wa pili msimu uliopita.
 “Hatujawahi kutishika dhidi ya timu yoyote ile, nadhani wao –Simba  wanajua Mtibwa ni timu ya aina gani na ili ujue ubora wako ni lazima  ucheze na aliye bora na upate matokeo,” anasema Barnabas akiwa Turiani,  Morogoro  siku ya leo Jumatatu.
 “Naamini tutapata matokeo mazuri. Tulipoteza mchezo wa kwanza katika  uwanja wa Uhuru kwa sababu moja kubwa, wakati ule tunakuta wachezaji  wetu wengi muhimu waliokuwepo msimu uliopita walihama. Timu ilikuwa  ikijijenga upya na kama umeiona timu yetu hivi sasa hauwezi kusema  tunashindwa. Naimani tutapata matokeo.” Anasisitiza mchezaji huyo wa  zamani wa Taifa Stars na vilabu vya Kagera Sugar na Yanga SC.
 Salum Mayanga ambaye aliisimamia Mtibwa kama kocha mkuu katika  michezo iliyopita ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa  Stars’ lakini kuondoka kwake hakujapunguza morari ya timu hiyo ikiwa  chini ya Zubery Katwila na Patrick Mwangata.
 “Morai ipo juu, na kama unavyojua makocha wetu wa sasa  Zubery  Katwila na Patrick Mwangata wapo hapa kwa muda mrefu sana. Ni sehemu ya  familia yao kwa miaka mingi hivyo wanajua Mtibwa inahitaji nini kwa  sasa. Mechi itakuwa nzuri na mashabiki waje kwa wingi kutazama  burudani.”
‘Hatujawahi kuihofia timu yoyote, tutapata ushindi vs Simba’ – Barnabas
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
 


No comments:
Post a Comment