Nyayo zilizoachwa na binadamu wa kale mamilioni ya miaka iliyopita zimegunduliwa nchini Tanzania karibu na pahala ambapo nyayo sawa na hizo ziligunduliwa miaka ya 1970.
Alama hizo za miguu ziliachwa na binadamu wa kale walipotembea kwenye matope na majivu ya volkano yaliyokuwa hayajakauka.
Wataalamu wanakadiria kwamba viumbe ambao hujulikana kama Australopithecus afarensis, ndio walioacha nyayo hizo, na walikuwa na kimo na unene uliotofautiana.
Wanasayansi wanasema nyayo hizo zinaashiria jinsi binadamu wa kale walivyoishi.
Australopithecus afarensis ni miongoni mwa aina ya binadamu wa kale wanaofahamika zaidi na ambao waliishi kipindi kirefu.
Visukuku vya "Lucy", mwanamke kijana aliyeishi Ethiopia zaidi ya miaka 3.2 milioni, ndiye maarufu zaidi kutoka kwa kundi hilo la binadamu.
Nyayo hizo zilizogunduliwa huenda ziliachwa na mwanamume aliyekuwa labda anatembea na wenzake wa kike wadogo kwa kimo.
"Ushahidi huu mpya, ukiuzingatia pamoja na ushahidi wa awali, unaashiria kwamba binadamu wa kale walikuwa wanatembea kama kundi kwenye mandhari ambapo kulikuwa na matope, majivu na mawe ya volkano baada ya kulipuka kwa volkano na mvua kunyesha. Lakini kuna zaidi," amesema mtafiti mkuu Prof Giorgio Manzi, mkurugenzi wa mradi huo wa akiolojia nchini Tanzania.
"Nyayo za mmoja wa binadamu kati ya zile tulizogundua ni kubwa kuliko za wengine katika kundi hilo, jambo linaloashiria kwamba huenda alikuwa mwanamume.
"Kusema kweli, kimo cha 165cm ambacho kinadokezwa na nyayo hizo kinamfanya kuwa moja wa binadamu wa Australopithecus warefu zaidi kugunduliwa hadi wa leo."
Maisha kama ya sokwe
Mwaka 1976, nyayo zilizohifadhiwa ambazo zinaaminika kuachwa naAustralopithecus ziligunduliwa karibu na Laetoli, kaskazini mwa Tanzania, takriban kilomita 40 kutoka Olduvai Gorge.
Nyayo hizo ambazo zinakadiriwa kuachwa miaka 3.66 milioni iliyopita, ni miongoni mwa nyayo za kale zaidi kugunduliwa duniani.
Sasa, ugunduzi wa kundi la sasa la nyayo umefichuliwa kwenye jarida la eLife.
Nyayo hizo ziligunduliwa wakati wa ufukuzi kwa ajili ya kujengwa kwa makumbusho eneo lililo mita 150 kusini mwa eneo ambalo ugunduzi wa kwanza ulifanywa.
Watafiti walioongoza uchunguzi huo, ambao wanatoka Italia na Tanzania, wanafikiri huenda nyayo hizo zina uhusiano, na zinaashiria mtindo wa maisha wa Australopithecus.
"Nadharia ambayo ni ya kuaminika ni kwamba kundi hilo labda lilikuwa na mwanamume mmoja, mwanamke mmoja au wawili au watoto, jambo ambalo linatufanya tuamini kwamba mwanamume huyo - alikuwa (alijamiiana) na wanawake zaidi ya mmoja," anasema Dkt Marco Cherin, mkurugenzi wa kitivo cha utaalamu wa mifupa ya kale katika Chuo Kikuu cha Perugia, Italia.
Ugunduzi huu unadokeza kwamba huenda mtindo wao wa kuishi ulikuwa "unakaribiana zaidi na wa sokwe kuliko sokwe-mtu au binadamu wa sasa," wanasema.
Miongoni mwa sokwe, sokwe dume na sokwe jike kadha huunda kundi la kujamiiana na kulea watoto.
Utafiti huo umeibua maswali kuhusu ni vipi na ni lini binadamu walipoanza kutembea wanavyotembea sasa.
Kutembea wima kwa miguu miwili
Australopithecus waliweza kutembea wakiwa wamesimama wima kwa miguu yao miwili, lakini hatujui walifanana kwa kiasi gani na binadamu wa sasa kwa jinsi walivyotembea.
Prof Robin Crompton wa Chuo Kikuu cha Liverpool, ambaye hakuhusika katika utafiti huo, anasema nyayo hizo zilizogunduliwa majuzi zitatoa maelezo zaidi, utathmini wa takwimu utakapofanyika.
"Baadhi ya watu wanasema walikuwa na mwendo tofauti kiasi, lakini sifikiri kwamba kuna ushahidi mzuri kuhusu hilo," ameambia BBC.
"Iwapo wanadamu wamekuwa wakitembea kwa mwendo sawa na wa sasa kwa zaidi au chini ya miaka 3.65 milioni, na mababu wa binadamu - katika kundi jingine la viumbe - Australopithecus - basi hilo linashangaza sana"
Asante kwa kutembelea Blog yetu washirikishe na wenzako,
Pia tunaomba maoni yako hapa au tupigie kwa (+255) 0769436440 Karibu Tena
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment