Trump awashutumu waliosherehekea kama Nazi
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amewashutumu vikali wafuasi wa kundi la mrengo wa kulia mabao walisherehekea ushindi wake kwa saluti ya Nazi.
Kwenye mahojiano ya kina na gazeti la New York Times la Marekani, rais huyo mteule amenukuliwa akisema: "Nawashutumu sana. Najitenga nao, na nawashutumu."
Alisema hataji "kuongeza nguvu" kundi hilo, ambalo linajumuisha wafuasi wa sera za Nazi, watu wanaotetea ubabe wa Wazungu pamoja na wanaopinga Wayahudi.
Nazi kilikuwa chama cha kisoshalisti kilichoongoza Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia, na kililaumiwa kwa kutekeleza mauaji dhidi ya Wayahudi.
Wafuasi wa makundi hayo walipigwa picha ya video Jumamosi mjini Washington DC wakishangilia, mtu mmoja kwenye kipaza sauti aliposema: "Hail Trump."
Nazi walimfurahia kiongozi wao Adolf Hitler kwa kuitikia "Heil Hitler' na "Heil, mein Fuhrer".
Kwenye video hiyo, Richard Spencer, kiongozi wa kundi moja la mrengo wa kulia, aliambia waliohudhuria kwamba Marekani ni ya watu weupe (Wazungu) pekee, ambao aliwaita "watoto wa jua".
Aliwashutumu wanaopinga kundi hilo akisema ndio "viumbe wabaya zaidi waliowahi kutembea katika sayari hii".
"Hail Trump, hail watu wetu, hail ushindi!" Spencer anasema wakati mmoja, huku baadhi ya waliohudhuria wakiinua mikono yao juu na kupiga saluti ya Nazi.
Mkutano huo wa Jumamosi uliwavutia waandamanaji walioziba barabara kuzunguka jumba la Ronald Reagan, jumba la mikutano linalomilikiwa na serikali katika mji huo mkuu wa Marekani.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alieleza wasiwasi Jumanne kwamba ushindi wa Bw Trump uchaguzini huenda ukawapa matumaini watu wanaoamini katika ubabe wa Wazungu.
- Familia ya Donald Trump: Wake na watoto
- Trump ajitokeza kwa kushtukiza mgahawani New York
- Watakaoumia na watakaofaidi chini ya Trump Marekani
Mmoja wa maafisa wake wakuu na wa karibu alisema video hiyo ya "Hail Trump" inaogofya.
Lakini Bw Trump ameendelea kumtetea mwanamikakati wake mkuu Steve Bannon, afisa mkuu mtendaji wa zamani wa Breitbart News, na akakosoa madai kwamba tovuti hiyo ya kihafidhina ina uhusiano na kundi hilo linalopigania ubabe wa Wazungu.
"Breitbart ni tovuti tu. Wanaandika habari kama vile tu nyinyi pia huandika," ameambia New York Times.
"Kama ningefikiria kwamba yeye ni mbaguzi wa rangi au kwamba anafuata mlengo wa kulia au baadhi ya hayo mambo, maneno ambayo tunaweza kutumia, hata singefikiria kumpa kazi," Bw Trump alisema kumhusu Bw Bannon.
Kwenye mahojiano yake na New York Times, rais huyo mteule alizungumzia mambo mengi yakiwemo:
- Shemeji yake Jared Kushner, mfanyabiashara wa nyumba na makao ambaye hana ujuzi katika demokrasia, anaweza kusaidia kupatikana kwa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina, alisema. Bw Kushner ni mumewe Ivanka, bintiye Bw Trump na ni Myahudi.
- Marekani haifai kuwa "mjenzi wa mataifa" duniani, alisema.
- Viongozi wa Republican Paul Ryan na Mitch McConnell "wanampenda tena, alisema
- Anaweza kuendesha biashara zake na nchi pia, bila kuwa na mgongano wa maslahi
- Kuna uhusiano fulani kati ya shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi
Mapema Jumanne, msemaji wa Bw Trump alisema kiongozi huyo hatafuatilia sana ahadi yake ya kuanzishwa kwa uchunguzi mpya kuhusu kashfa ya barua pepe ya aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Mshauri wake alisema rais huyo mteule hatamteua mwendesha mashtaka maalum wa kumchunguza Bi Clinton, na kwamba kuachwa kwa suala hilo kutamsaidia "kupona".
Baadaye, bw Trump alinukuliwa akiambia New York Times: "Sitaki kuumiza familia ya Clinton, sitaki kamwe.
"Alipitia mengi na ameumia kwa njia nyingi kuu tofauti."
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment