» »Unlabelled » Serikali Kutoa Ajira Mpya 71,496 Hivi Karibuni

Serikali Kutoa Ajira Mpya 71,496 Hivi Karibuni

SERIKALI imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,

“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.

Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.

Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 16.

“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.

Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.

Alisema upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.

Pia alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.

Alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.

“Baada ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira. 

"Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200 kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.

“Katika malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.

Pia aliwaagiza maofisa utumishi kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.

“Mtu yeyote ambaye anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.

Pakua App Yetu-Bofya Hapa Flower
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

About 4sn News

Hi my name is Gasto Alex Didas from Mwanza Tanzania I'm blog manager and I have an App which is called 4sn News, my office is located in Rock City Mwanza-Tanzania at Miembeni "B" Street. My contacts +255769436440/ +255659750504 Welcome.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Popular Articles

MBUNGE MABULA AKAGUA SHULE NNE MPYA ZA MSINGI, ZENYE THAMANI YA TSH 1.174 BIL, ASHAURI HALMASHARI KUTUMIA MCHORO MPYA WA TAMISEMI KUOKOA MADARASA 3 KILA SHULE

Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo La Nyamagana amefanya ziara ya kikazi katika Kata nne za halmashauri ...