Je, Simu za Mkononi Zina Faida au Hasara?
MIAKA kadhaa iliyopita, ungeweza
kutumia simu ya mkononi ikiwa ulikuwa na nguvu za kuibeba au ikiwa
ilikuwa imeunganishwa na mfumo wa gari lako, kwani betri zake zilikuwa
nzito sana. Simu hizo zilikuwa kubwa kuliko boksi za viatu, nazo
ziligharimu maelfu ya dola.
Leo kuna simu za mkononi bilioni 1.35
hivi. Katika nchi fulani, zaidi ya nusu ya wakaaji wana simu hizo. Simu
nyingi za mkononi zinaweza kutoshea kwenye kiganja cha mkono wako, na
nyakati nyingine unaweza kupewa simu ya mkononi bila malipo.* Jarida The Bulletin la
Australia linaripoti hivi: “Idadi ya simu za mkononi zinazotumiwa
inakaribia jumla ya idadi ya televisheni na kompyuta.” Katika nchi zaidi
ya 20, idadi ya simu za mkononi inapita idadi ya simu za waya. Mtaalamu
mmoja alisema kwamba zaidi ya kuwa hatua kubwa ya kiteknolojia, simu za
mkononi “zimebadili jamii.”
Zinafaidi Biashara
Biashara nyingi zinafaidika kwa kuwa
simu nyingi za mkononi zinauzwa. Shirika moja kubwa lilisema hivi: “Simu
ya mkononi ndicho kifaa cha elektroni kinachouzwa kwa wingi zaidi.”
Basi, leo watu wanatumia pesa nyingi zaidi kununua simu za mkononi
ikilinganishwa na pesa walizotumia zamani kununua kifaa chochote kile
cha elektroni.
Kwa mfano, zaidi ya watu milioni 15
kati ya wakaaji milioni 20 wa nchi ya Australia wana simu za mkononi.
Katika kipindi cha mwaka mmoja hivi majuzi, wateja wa kampuni moja ya
simu za mkononi kati ya kampuni nyingi za simu zilizo nchini humo
walipiga simu bilioni 7.5. Kampuni za simu ulimwenguni hupata mabilioni
ya dola kwa mwaka kutokana na simu za mkononi. Basi si ajabu kwamba
makampuni makubwa huona simu za mkononi kuwa zenye faida.
Kubuni Lugha Mpya
Mara nyingi watu wanapowasiliana
kwa simu za mkononi hawazungumzi bali wao huandika ujumbe. Badala ya
kuzungumza kwa simu, watu wengi wanaotumia simu za mkononi, hasa vijana,
hutuma ujumbe mfupi. Kwa njia hiyo, wao huandika na kutumiana ujumbe
mfupi kwa bei nafuu. Kwa kuwa mawasiliano hayo huhusisha kuandika ujumbe
kwa kutumia vibonyezo vidogo vya simu, wale wanaofanya hivyo hufupisha
maneno kwa kuchanganya herufi na nambari ili kutokeza ujumbe unaoweza
kutamkwa. Ijapokuwa njia hiyo ya kuwasiliana si rahisi ikilinganishwa na
kuzungumza kwa simu, kila mwezi ujumbe bilioni 30 hutumwa ulimwenguni
pote.
Ni habari gani zinazotumwa kupitia
simu hizo? Uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Uingereza ulionyesha kwamba
asilimia 42 ya vijana kati ya umri wa miaka 18 na 24 hutuma ujumbe
mfupi kwa simu ili kuchezeana kimapenzi, asilimia 20 hutuma ujumbe ili
kupanga kukutana na watu wa jinsia tofauti, na asilimia 13 wametuma
ujumbe ili kuvunja uhusiano.
Baadhi ya watu wanaochunguza hali
za kijamii wanahofu kwamba njia ya kuandika maneno na lugha inayotumiwa
katika ujumbe mfupi inaathiri uwezo wa lugha wa vijana. Wengine
hawakubaliani na maoni hayo kwani wanasema kwamba njia hiyo ya
kuwasiliana “imechochea tena upendezi wa kuandika katika kizazi kipya.”
Msemaji wa shirika ambalo hutayarisha kamusi moja ya Kiaustralia
aliliambia gazeti Sun-Herald hivi: “Si kawaida kupata nafasi ya
kubuni [lugha] mpya . . . ujumbe wa simu na intaneti huwafanya vijana
waandike sana. Inawabidi wawe wenye ufasaha ili watambue na kujifunza
maneno . . . yanayotumiwa sana.”
Mambo Fulani Yasiyopendeza
Ingawa simu ya mkononi ni kifaa
chenye faida katika mawasiliano ya kirafiki na ya kibiashara, kifaa
hicho huwafanya wafanyakazi wengi wahisi kwamba wamefungiwa ofisini.
Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 80 ya watu wanaofanya
matangazo ya biashara na asilimia 60 ya wajenzi huona ni lazima wawe na
simu za mkononi kila wakati ili wapokee simu kutoka kwa waajiri au
wateja wao. Watu huona ni lazima wapokee simu haidhuru wako wapi au
wanafanya nini, na mtafiti mmoja alifafanua tabia hiyo kuwa “tabia ya
mvurugo.” Ili kukabiliana na tatizo hilo, wataalamu wa mambo ya ujenzi
wamebuni kifaa cha ujenzi kinachoweza kuzuia mawimbi ya redio ya simu za
mkononi kitakachotumiwa katika kujenga mikahawa na majumba ya
sinema.—Ona sanduku “Madokezo ya Kutumia Simu ya Mkononi.”
Zaidi ya kuwavuruga watu, simu za
mkononi zinaweza kuhatarisha umma. Uchunguzi uliofanywa huko Kanada
ulionyesha kwamba kutumia simu ya mkononi unapoendesha gari ni hatari
sana kama vile kuendesha gari ukiwa umekunywa kileo. Profesa Mark
Stevenson, wa Kituo cha Utafiti wa Majeraha katika Chuo Kikuu cha
Western Australia, anasema kwamba ni vigumu kuzungumza na mtu kwa simu
unapoendesha gari kuliko kuzungumza na mtu aliye ndani ya gari hilo.
Licha ya hatari hizo na uwezekano wa kutozwa faini na polisi, uchunguzi
uliofanya hivi karibuni ulionyesha kwamba dereva 1 kati ya madereva 5
huko Australia alituma ujumbe mfupi wa simu na thuluthi moja walipiga au
kupokea simu walipokuwa wakiendesha gari.
Usafiri wa ndege pia unaathiriwa na
matumizi mabaya ya simu za mkononi. Ijapokuwa nyaya za ndege za kisasa
zimekingwa zisiathiriwe na mawimbi ya redio ya simu za mkononi, ndege za
zamani zinaweza kuathiriwa. Gazeti New Scientist linaripoti:
“Majaribio yaliyofanywa katika ndege mbili na Shirika la Usafiri wa
Ndege la Uingereza yamethibitisha kwamba mawimbi ya simu za mkononi
huathiri mitambo muhimu ya ndege.” Msemaji mmoja wa shirika hilo
alionyesha hatari moja kubwa inayosababishwa na simu za mkononi
aliposema hivi: “Simu ya mkononi hutoa nguvu nyingi zaidi kadiri
inavyokuwa mbali na kituo cha kurusha na kupokea mawimbi. Hivyo, kadiri
ndege inavyozidi kupaa ndivyo mawimbi ya simu yanavyozidi kuwa na nguvu
na hilo huathiri zaidi mitambo ya ndege wakati muhimu sana.” Uchunguzi
mmoja uliofanywa huko Australia ulionyesha kwamba katika visa kadhaa
vifaa vya elektroni vinavyotumiwa na watu binafsi, kutia ndani simu za
mkononi, viliathiri mitambo ya ndege zilipokuwa hewani kwa sababu abiria
walipuuza maonyo ya kuzima vifaa hivyo walipokuwa ndani ya ndege.
Bado kuna maoni tofauti-tofauti
kuhusu ikiwa mawimbi ya redio yanayotoka katika simu za mkononi na vituo
vya kupokea na kurushia mawimbi hayo yanaweza kuwafanya watu wapate
kansa. Kwa kuwa watu wengi sana hutumia simu hizo, hata asilimia ndogo
kati yao wakiathiriwa, hilo linaweza kuwa tatizo kubwa la afya. Hivyo,
utafiti mwingi wa kisayansi umefanywa ili kuchunguza ikiwa mawimbi ya
simu za mkononi huathiri chembe za mwili. Utafiti huo umeonyesha nini?
Kikundi fulani cha wataalamu
wanaochunguza simu za mkononi kilitoa ripoti iliyosema: “Kikundi hiki
kinaamini kwamba kwa msingi wa uthibitisho uliopo, watu hawapaswi
kuhangaika kuhusu matumizi ya simu za mkononi.” Pia gazeti New Scientist liliripoti
hivi: “Licha ya habari zenye kuogopesha katika miaka ya karibuni,
uthibitisho mwingi uliopo unaonyesha kwamba mawimbi ya redio ya simu za
mkononi hayaathiri afya ya mtu. Uchunguzi ambao umeonyesha athari fulani
haukuweza kuthibitishwa uliporudiwa.”
Kwa kuwa kuna mashaka kuhusu athari
za afya zinazosababishwa na simu za mkononi, mamilioni ya dola
zinaendelea kutumiwa kufanya uchunguzi. Kabla ya habari kamili
kupatikana, kikundi hicho cha wataalamu kinapendekeza hivi: “Tumia simu
[za mkononi] kwa muda mfupi iwezekanavyo. Tumia simu zinazotoa kiwango
kidogo cha mawimbi ya redio. Tumia vifaa vinavyokuwezesha kutumia simu
bila kuishika maadamu imethibitishwa kwamba vinapunguza kiwango cha
mawimbi.” Pia kikundi hicho cha wataalamu kinapendekeza kwamba “watoto
walio na umri wa chini ya miaka kumi na sita wasiruhusiwe kutumia simu
za mkononi,” kwani “ni rahisi kwao kuathiriwa kiafya na matatizo
yasiyojulikana” kwa kuwa mfumo wao wa neva unaendelea kukua.
Licha ya maoni tofauti-tofauti,
simu za mkononi zinabadili sana uchumi na hali ya jamii. Sawa na vifaa
vingine vya elektroni kama vile televisheni na kompyuta, tunaweza
kutumia simu za mkononi vizuri au tunaweza kuziruhusu zitutawale. Uwezo
wa kutumia simu za mkononi kwa faida au kwa hasara umo mikononi mwetu.
[Maelezo ya Chini]
Nyakati nyingine
simu za mkononi hutolewa bila malipo kwa wale wanaokubaliana na shirika
la kutoa huduma za simu za mkononi kwamba watatumia kiasi fulani cha
pesa katika kipindi fulani hususa.
1. Usizungumze kwa
sauti ya juu unapozungumza kwa simu ukiwa katika maeneo ya umma.
Maikrofoni ya simu ya mkononi ina uwezo mkubwa wa kupokea sauti, na watu
walio karibu nawe hawahitaji kusikiliza mazungumzo yako ya siri.
2. Zima simu yako,
au utumie mfumo wa kutetema badala ya kutoa mlio unapokuwa kwenye
mikutano ya kidini au ya kibiashara, unapokuwa katika jumba la sinema,
katika mkutano mwingine wowote wa umma, au mkahawani.
3. Usitumie simu kwa kuishika mkononi unapoendesha gari.
Ulimwenguni pote, ujumbe bilioni 30 hutumwa kila mwezi kupitia simu za mkononi
Kutumia simu ya mkononi unapoendesha gari ni hatari sana kama vile kuendesha gari ukiwa umekunywa kileo
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment