Malecela: Kupona kwangu ni miujiza ya Mungu
Waziri Mkuu na Makamu wa Rais wa zamani Dk John Malecela, amesema haamini ni kwa namna gani alivyotendewa miujiza na Mungu hadi kuendelea kuwa hai hadi sasa.
Malecela ametoa kauli hiyo Aprili 8 muda mfupi baada ya ibada ya shukrani kwa Mungu ambako aliongozana na familia yake, wabunge, wazee wa Dodoma na watu maarufu kwa ajili ya kushukuru kanisani kutokana na afya yake kuimarika.
“Kwanza namini hakuna binadamu ambaye aliwahi kufumuliwa mwili wake kama ilivyotokea kwangu mimi kati ya wote waliojaa ndani ya kanisa hili, nasema ni Mungu pekee tu na wala si kitu kingine,” amesema Malecela
Mzee huyo amesema kuwa katika uhai wa maisha yake alipitia katika shida kubwa ambayo awali hakuwa anaijua lakini ghafla alijikuta akipasuliwa mwili wake na kufumuliwa zaidi ili kuurudisha katika yake.
Amesema ni jambo jema kumshukuru Mungu kwa kila hali kwani ndiye anayewezesha kila jambo na bila mkono wake hali ingekuwa ni ngumu zaidi.
Akitoa neno la shukrani kanisani jana, mtoto mkubwa wa Malecela Dk Mwele Malecela amesema kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alipitia katika vipindi vigumu zaidi kaika afya yake.
Dk Mwele amesema baba yake alifanyiwa upasuaji mkubwa mara tatu ambapo tatizo la moyo alifanyiwa upasuaji mara mbili na kisha akapasuliwa tena kuhusu tatizo la mgongo.
“Yote hayo yalifanyika katika kipindi cha miaka michache, leo hii tunapomuona mzee anaimarika na kuwa na afya nje kwetu sisi ni jambo la kushukuru na ndiyo maana tumeona tuje tuseme asante Mungu,” amesema Dk Mwele
Awali Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dk Dickson Chilongani amesema hakuna mtu aliyemkubwa mbele za Mungu na wala hakuna mwenye cheo cha kumshinda Mungu.
Dk Chilongani amesema jambo kubwa ni kwa kila mmoja kuendelea kujishusha na kujinyenyekeza mbele za Mungu wakai wote ili Mungu awe zaidi ya wote maana ndiye mgawaji mwema.
Askofu huyo aliwataka Watanzania kuendelea kuilinda amani ya taifa ili iweze kudumu na kuliepusha taifa kuingia katika machafuko kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani.
Kuhusu Malecela, alimshukuru kwa uamuzi wake pamoja na michango mikubwa aliyotoa ikiwemo kusaidia ujenzi wa kanisa katika Kijiji cha Chinangali II ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya shukrani zake mbele za Mungu na jana aliongoza utoaji wa sadaka kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya utumishi katika kanisa hilo lililoko kijijini.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment