» » Jeshi la Polisi Lasema Linawashikilia Watu 3 Kwa Kuvamia Mkutano wa CUF na Kuwapiga Watu

Jeshi la Polisi Lasema Linawashikilia Watu 3 Kwa Kuvamia Mkutano wa CUF na Kuwapiga Watu

Saa  tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza kushikilia watu watatu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona  Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.

Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.

Jumamosi iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.

Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.

“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.

Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”

Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni  wakapatanishwe.

“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.

Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.

“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.

Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.

Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.

Tuma picha/ habari what-sap 0769436440

BONYEZA HAPA KUPATA APP YA 4SN NEWS

tupe maoni yako

Pakua App Yetu-Bofya Hapa Flower
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

About 4sn News

Hi my name is Gasto Alex Didas from Mwanza Tanzania I'm blog manager and I have an App which is called 4sn News, my office is located in Rock City Mwanza-Tanzania at Miembeni "B" Street. My contacts +255769436440/ +255659750504 Welcome.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Popular Articles

MBUNGE MABULA AKAGUA SHULE NNE MPYA ZA MSINGI, ZENYE THAMANI YA TSH 1.174 BIL, ASHAURI HALMASHARI KUTUMIA MCHORO MPYA WA TAMISEMI KUOKOA MADARASA 3 KILA SHULE

Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo La Nyamagana amefanya ziara ya kikazi katika Kata nne za halmashauri ...