Yote Katika Mpango wa Mungu
Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu Ayubu 28:28.
Maisha ya Yusufu ya kupanda na kushuka, hayakuja kwa ajali; yalikuwa yamepangwa na Mungu. Lakini aliwezaje kuweka rekodi ya namna hiyo ya uthabiti katika tabia, unyofu na hekima? Haya yalikuwa ni matokeo ya mafunzo yaliyofanyika kwa uangalifu katika miaka yake ya awali. Alikuwa ameona wajibu badala ya hisia; na uadilifu, kuaminika katika maisha ya kawaida, tabia ya uungwana ya ujanani ilizaa matunda katika matendo ya mwanamume huyu. Talanta zilizo nzuri sana hazina thamani kama hazikuzwi; mazoea ya kufanya kazi kwa bidii na nguvu ya tabia lazima vipatikane kwa kuvikuza. Tabia ya hali ya juu ya kimaadili na hali nzuri ya kiakili haviji kama ajali. Mungu anatupa fursa; mafanikio yanategemea namna tunavyozitumia. Nafasi zinazotolewa na Mungu lazima zionekane kwa haraka na zishikiliwe kwa shauku.
Mungu alijidhihirisha mwenyewe kupitia kwa Yusufu, sio kwa watu wa Misri peke yake, bali pia kwa mataifa yote yaliyounganika na taifa lile kubwa. Alitamani kumfanya kuwa mbeba nuru kwa watu wote na hivyo akamweka karibu na kiti cha enzi cha ufalme mkuu kabisa katika dunia ili mwangaza wa kimbingu upate kwenda mbali na karibu.
Wapo wachache wanaotambua mvuto wa mambo madogo ya maisha katika maendeleo ya tabia. Kati ya yote tunayofanya hakuna lililo dogo kwa kweli. Mazingira anuai tunayokutana nayo siku kwa siku yamepangwa kwa ajili ya kupima uaminifu wetu na kutufanya tufae kwa ajili ya kuaminiwa na mambo makubwa zaidi. Kwa kushika kanuni katika shughuli za kawaida za maisha, akili inazoea kushikilia yanayohitajika katika majukumu kuliko yale ya starehe na ya hisia. Akili zilizonidhamishwa kwa namna hiyo haziyumbi kati ya makosa na yaliyo sahihi, kama jani linavyotetemeka kwenye upepo; huwa wanakuwa watii kwa wajibu kwa sababu wamejifunza mazoea ya uaminifu na ukweli. Kwa kuwa waaminifu katika kile kilicho kidogo wanapata nguvu ya kuwa waaminifu katika yale yaliyo makubwa. Tabia ya uaminifu ni ya thamani kubwa kuliko dhahabu ya Ofiri. Bila ya hiyo, hakuna mtu atakayeweza kuinuka na kufikia heshima iliyo kuu. Lakini tabia hairithiwi. Haiwezi kununuliwa. Ubora wa kimaadili na uzuri wa kiakili hauji kama matokeo ya ajali. Karama za thamani sana hazina thamani kama zisipoboreshwa.
No comments:
Post a Comment