NA FLORENCE SANAWA – MTWARA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limebaini wizi wa umeme katika nyumba ya aliyekuwa Mbunge wa Mtwara Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hasnain Murji.
Mhandisi wa Tanesco Mkoa wa Mtwara, Fabiani Ruhumbika, alisema mita ya nyumba ya Murji ilibainika kuchezewa baada ya kuona umeme unaotoka kwenda kwa mteja ni kidogo.
Alisema matumizi ya mteja yanaonekana kuwa ni makubwa kuliko kiasi kinachotumiwa hali iliyowatia shaka kwamba kutakuwa na kuchezewa kwa mita.
Ruhumbika alisema kitendo cha mteja kupindisha mita kutoka kushoto kwenda kulia inaonyesha wazi kuwa ilipoteza kumbukumbu katika usomaji wake.
Mwakilishi wa mbunge huyo wa zamani, Mohamed Haji, alisema kitendo cha kubaini wizi huo hakijui kwa sababu yeye hana ufahamu wa masuala ya umeme.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Murji kwa simu, alisema hakuwa na taarifa ya tukio hilo
Akizungumza mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Ukaguzi wa Miundombinu ya Umeme kutoka Makao Makuu ya Tanesco, John Manyama, alisema wizi huo umekuwa ukilirudisha nyuma shirika hilo na kufifisha mipango yake ya kujiendesha.
Alisema ukaguzi huo ulibaini kuwapo na uchezewaji mita katika nyumba hiyo, huku kukiwa na vifaa vingi vinavyotumia umeme.
Manyama alisema wataalamu wa ukaguzi waligundua wizi wa umeme huo kutokana na kutumia vifaa vya kisasa vya kupimia bila kumwonea mtumiaji wa huduma hiyo.
Alisema mtumiaji anayekamatwa huanza kwa kukatiwa umeme katika mtandao wa Tanesco kisha wanapiga hesabu ili kujua wamepoteza kiasi gani cha fedha na kumtaka kulipa.
“Tumebaini kuwa watu wengi wanatumia umeme bila kulipa (wezi wa umeme) hatua inayosababisha shirika kuchukua hatua kwa kuwakamata na kuwapeleka katika vyombo vya sheria ili kuruhusu liweze kukusanya mapato halisi na kuwa katika hali nzuri ya utoaji wa huduma.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment