Kiungo mwenye kasi wa Yanga, Simon Msuva amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia wanaanza rasmi mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kukutana na Majimaji.
Kauli hiyo ya Msuva imekuja baada ya timu hiyo kulikosa taji la ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ambayo Yanga iliondolewa na Simba kwenye hatua ya nusu fainali.
Yanga, wanatarajiwa kupambana na Majimaji, Januari 17, mwaka huu mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Songea.
Msuva alisema mashabiki wasikate tamaa baada ya kulikosa Kombe la Mapinduzi na badala yake wanachotakiwa kukifanya ni kuungana kwa pamoja ili wautetee ubingwa wao wa ligi kuu.
Msuva alisema michuano hiyo waliichukulia kama sehemu ya maandalizi ya ligi kuu, hivyo haumizwi na kuukosa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Alisema michuano hiyo imewasaidia kujua upungufu wa kikosi chao ambao Kocha George Lwandamina kwa kushirikiana msaidizi wake Juma Mwambusi wataufanyia marekebisho ili wapate matokeo mazuri katika ligi.
“Ninaamini kocha amejua upungufu wa kikosi chetu baada ya kuondolewa na Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
“Hicho ndicho tulichokuwa tunakihitaji kwa kupitia Kombe la Mapinduzi ni kujua upungufu wetu ambao kocha ataufanyia marekebisho kwa kuziboresha sehemu zenye upungufu tukijiandaa kucheza na Majimaji.
“Mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuachana na maneno ya kejeli na vijembe wanayoyapata kutoka kwa wapinzani wetu, nikwambie tu tumepanga kulitetea taji letu la ligi kuu,” alisema Msuva.
SOURCE: CHAMPIONI
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment