» » Atumia jina la Waziri kumiliki Ziwa

MKAZI wa Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, Richard Mwananzila anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kujimilikisha Ziwa Sundu lililopo katika Kata ya Sundu Wilaya ya Kalambo, huku akiwatisha wavuvi kuwa yeye ni mtoto wa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba.
Amri ya kukamatwa kwake ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, ambaye alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD) kumsaka mtu huyo kwa udi na uvumba na kumfikisha mahakamani.
 
Mbali ya kujimilikisha Ziwa, Mwananzila anashutumiwa pia kwa kuuza zana haramu za uvuvi na kuwatapeli wavuvi fedha zao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mtu huyo huwatishia wavuvi wanaovua katika ziwa hilo kutovua bila kumpa fedha kwa vile ziwa hilo ni mali yake na kuwataka pia kununua zana haramu za uvuvi kutoka kwake na wanaogoma huwazuia akisema yeye ni mmiliki halali wa ziwa hilo.
“Kama vile haitoshi nimeelezwa pia kuwa mtu huyu anajigamba kuwa hakuna kiongozi yoyote wa serikali mwenye ubavu wa kumkamata kwa kuwa yeye ni mtoto wa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Pamoja na kuagiza kukamatwa kwake haraka, Binyura pia alitoa amri ya kuteketezwa kwa zana haramu za uvuvi za mfanyabiashara huyo zilizokakamatwa kufuatia doria maalumu zilizofanyika katika ziwa hilo na zile zilizokamatwa katika Kijiji cha Kasanga kilichopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo.
Aidha aliwaagiza askari wa kikosi cha doria kuendelea kuwasaka wavuvi wengine wanaotumia zana haramu za uvuvi na kuteketeza raslimali zinazopatikana katika Ziwa Sundu na Ziwa Tanganyika yaliyopo wilayani humo kwa kufanya doria za mara kwa mara na za kushtukiza.
“Nakuagiza OCD wa Kalambo hakikisha mfanyabiashara huyu (Mwananzila) atatafutwa popote pale alipo mkamateni ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. “Isitoshe nawaagiza askari wa kikosi cha doria muendelee kuwasaka wavuvi wanaotumia zana haramu za uvuvi kwa kufanya doria za mara kwa mara na za kushtukiza ili kuzilinda raslimali zilizopo katika Ziwa Sundu na Ziwa Tanganyika,“ aliaagiza.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutoandikwa gazetini kutokana na kumuhofia Mwananzila, baadhi ya wavuvi walidai wanamfahamu mfanyabiashara huyo kuwa ni mkazi wa Sumbawanga mjini.
“Huyu mfanyabiashara anaitwa Richard Mwananzila ni mkazi wa mjini Sumbawanga amekuwa akitutishia sisi wavuvi wageni tunaomiliki leseni za uvuvi kwamba tusiponunua zana haramu za uvuvi kutoka kwake basi hataturuhusu kuvua samaki katika Ziwa lake la Sundu kwa kuwa ana hati miliki yote ya ziwa hilo huku akitishia kuwa yeyote atakayemfuatilia atakiona cha moto kwa kuwa ni mtoto wa Waziri Dk Tizeba,” alisema mmoja wa wakazi hao akiwa na hofu kubwa ya kugunduliwa.
Awali, akitoa taarifa ya uvuvi haramu katika kipindi cha mwaka 2016/2017 katika kituo cha doria kilichopo kijijini Kasanga katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika, Ofisa Mfawidhi Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi na Udhibiti, Ubora wa Mazao ya Uvuvi wa Wilaya ya Kalambo Msabaha Kashindi alimweleza Mkuu wa Wilaya Binyura juu ya kuwepo kwa mfanyabiashara anayedaiwa kuwa mtoto wa Dk Tizeba.
Kashindi alimweleza DC kuwa wakati wakifanya doria waligundua uharibifu mkubwa wa mazingira katika Ziwa Sundu kwa kuwepo kwa idadi kubwa za nyavu haramu za uvuvi ambapo walipowakamata wavuvi haramu katika mahojiano nao walidai kuwa wanauziwa nyavu hizo na mfanyabishara aitwaye Mwananzila.
“Wavuvi hao haramu walidai kuwa mfanyabiashara huyo wa zana hizo haramu za uvuvi alijitambulisha kwao kuwa ni mtoto wa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwamba amepewa hatimili ya ziwa hilo na hakuna wa kumsumbua,“ alieleza Kashindi.
Kwa upande wake , Diwani wa Kata ya Sundu Peter Simuyemba alithibitisha kuwepo kwa taarifa za Mwananzila na kusema kuwa amekuwa tishio kutokana na kuaminiwa kuwa ni mtoto wa waziri anayemiliki ziwa kihalali.
“Juzi usiku alinipigia simu akinitishia maisha akinituhumu kuwa nimewaleta askari wa doria wa kanda ambao wanafanya doria katika Ziwa lake la Sundu. “Aliniambia kwamba nimekuwa nikimwaribia biashara yake na nitamtambua yeye ni nani. Nilipoona namba yake ya simu kabla ya kupokea simu nikaiseti na ikaanza kurekodi mazungumzo yetu, baadaye nikamtaarifu ofisa mwandamizi wa uvivu, na maelezo yapo, “ alieleza diwani.
Akifafanua alieleza kuwa akishirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sundu wameshataarifu polisi juu ya kutishiwa maisha na mfanyabiashara huyo lakini bado hajakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Pakua App Yetu-Bofya Hapa Flower
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

About 4sn News

Hi my name is Gasto Alex Didas from Mwanza Tanzania I'm blog manager and I have an App which is called 4sn News, my office is located in Rock City Mwanza-Tanzania at Miembeni "B" Street. My contacts +255769436440/ +255659750504 Welcome.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Popular Articles

MBUNGE MABULA AKAGUA SHULE NNE MPYA ZA MSINGI, ZENYE THAMANI YA TSH 1.174 BIL, ASHAURI HALMASHARI KUTUMIA MCHORO MPYA WA TAMISEMI KUOKOA MADARASA 3 KILA SHULE

Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo La Nyamagana amefanya ziara ya kikazi katika Kata nne za halmashauri ...