» »Unlabelled » LESSONI YA WIKI HII Somo la 1: Mwisho

Somo la 1: Mwisho Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu (Ayubu 31, 38-42) Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza. Utangulizi: Mwisho? Kwa nini unaanza somo jipya katika kitabu cha Ayubu na kulipa somo la kwanza kichwa cha habari kuwa, “Mwisho?” Muulize mke wangu. Anapokuwa anasoma kitabu, huwa anaanza kwa kusoma mwisho wa kitabu. Kamwe sijawahi kufanya hivyo, lakini mke wangu huwa anataka kufahamu jinsi mambo yatakavyokuwa kwa sababu kwa kufanya hivyo huwa anapata faraja anapokuwa anaendelea kusoma kitabu. Kutokana na utamaduni wa mke wangu, hebu tuzame kwenye somo kutoka katika kitabu cha Ayubu kwa kuuangalia mwisho wake! I. Mtazamo wa Ayubu Juu Yake na Juu ya Haki A. Kwa kuwa tunaanzia mwisho wa kitabu, ngoja nikupe kwa ufupi yaliyomo katika kitabu cha Ayubu. Ayubu ni mtu wa muhimu sana aliyebarikiwa na Mungu. Hata hivyo, katika mfululizo wa matukio ya kutisha, anapoteza kila kitu, ikiwa ni pamoja na afya yake. Swali la msingi katika kitabu hiki ni “Kwa nini?” B. Soma Ayubu 31:1. Anayezungumza hapa ni Ayubu. Anazungumzia nini kuhusu usafi wake wa masuala ya ngono? (Kwamba kwa makusudi anakataa kuwaangalia wanawake kwa kuwatamani.) C. Soma Ayubu 31:2-3. Jambo gani linapaswa kuwa matokeo ya huu usafi? (Mungu anapaswa kuwaangamiza waovu, na sio wema. Ayubu anauliza kuwa, inawezekanaje mambo mabaya yanananitokea, ikiwa Mungu yu makini?) 1. Yakobo anapozungumzia “sehemu ya Mungu itokayo juu” na “urithi wake,” je, anazungumzia nini kuhusu wajibu wa Mungu? (Zawadi ya Mungu kwa wanadamu ni kwamba wale wanaotenda makosa wanateseka.) a. Ni kwa jinsi gani jambo hilo ni zawadi, urithi? (Ukiepuka kutenda mabaya, mambo mabaya hayatakutokea – sasa hiyo ndio zawadi. D. Soma Ayubu 31:5-6. Ayubu analeta madai gani mengine kuhusu tabia yake njema? (Kwamba yeye ni mwaminifu.) E. Soma Ayubu 31:9-11. Ayubu anauzungumziaje mwenendo wake ikiwa ni pamoja na kutowatamani wanawake wengine? (Pia hakuwa akifanya nao mapenzi.) F. Soma Ayubu 31:13-15. Ayubu anasema kuwa mtazamo wake dhidi ya wale walio katika malango yake (watumishi wake) ukoje? (Anawatendea haki kwa sababu anafahamu kuwa yeye pamoja na watumishi wake lazima wawajibike kwa Mungu.) G. Soma Ayubu 31:16-18. Ayubu anawatendeaje maskini pamoja na watu wasio na uwezo? (Anawatendea kama anavyowatendea watoto wake.) H. Soma Ayubu 31:24-28. Ayubu alikuwa mtu tajiri sana. Je, mtazamo wake juu ya fedha ulikuwaje? 1. Alikuwa na mtazamo gani juu ya jua na mwezi? (Ayubu anadai kuwa hakuamini katika utajiri wala mbingu. Imani (matumaini) yake ilikuwa kwa Mungu.) I. Soma Ayubu 31:29-30. Ayubu ana mtazamo gani juu ya maadui wake? (Hafurahii pale wanapoanguka, na pia hawalaani.) J. Chukulia kwamba Ayubu anatuambia ukweli, je, kitendo hiki kinamzungumziaje? (Linapokuja suala la usafi, uaminifu, huruma, na kumtumaini Mungu, yeye ni mwaminifu.) II. Madai ya Ayubu ya Kutendewa Haki A. Soma Ayubu 31:35-37. “Utetezi,” “jibu,” “mashtaka” – maneno yote haya ni msamiati wa kisheria. Ayubu anasema nini? (Anataka mtu fulani awe hakimu kati yake na Mungu. Ayubu anasema, “Niko radhi kuwajibika kwa matendo yangu.” Ninataka mtu aliye mkuu zaidi ya Mungu kutoa uamuzi endapo nimekuwa mwaminifu au la.”) 1. Kwa nini Ayubu anataka kumshtaki Mungu? (Soma tena Ayubu 31:2-3. Watu wabaya ndio wanaotakiwa kuteseka, na si watu wema. Ayubu anasema “Ninafahamu kanuni za kimfumo, nimefanya kilicho sahihi. Mungu hakunitendea haki, Mungu hafuati kanuni zake. Niko radhi kuthibitisha kuwa nimekuwa mtiifu.”) 2. Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-2 na Kumbukumbu la Torati 28:15. Je, Ayubu hayuko sahihi kuhusu mfumo wa utendaji wa Mungu? (Hapana. Ayubu anafahamu jinsi ambavyo mfumo wa Mungu unatakiwa kufanya kazi.) B. Soma Ayubu 32:1. Je, tumekosea kile ambacho Ayubu anakijengea hoja? (Hapana. Watu watatu walio pamoja naye wanaelewa kwamba Ayubu anajenga hoja kuwa yeye ni mwenye haki na kile kinachomtokea si kitendo cha haki.) III. Majibu ya Mungu kwa Ayubu A. Soma Ayubu 38:1. Tunatakiwa kuwa na taswira gani kiasili tunaposoma kuwa Mungu anajibu “katika upepo wa kisulisuli?” (Mungu anatokea mahali penye uwezo mkubwa tena pa hatari.) B. Soma Ayubu 38:2-3. Je, Mungu anampa Ayubu mashtaka yake? (Ndiyo, kwa namna fulani. Mungu anasema kuwa atamuuliza Ayubu na Ayubu atatakiwa kutoa majibu.) 1. Mungu anamaanisha nini anaporejea “mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa?” (Anamaanisha kuwa Ayubu hafahamu taarifa zote za muhimu. Ayubu anadhani kuwa tabia yake na kanuni za jumla za Mungu ndio mambo pekee ya msingi, lakini Mungu anasema kuwa Ayubu amepungukiwa taarifa za muhimu.) C. Soma Ayubu 38:4-7. Mungu anamaanisha nini katika maswali yake kwa Ayubu? (Mungu aliuumba ulimwengu na Ayubu hakuumba.) D. Soma Ayubu 38:16-18. Mungu anamaanisha nini katika haya maswali? (Kwamba Ayubu haufahamu kwa kina ulimwengu wake mwenyewe. Mungu anaufahamu ulimwengu kwa kina, kuanzia nje hadi ndani kabisa.) E. Soma Ayubu 38:19-21. Mungu anamaanisha nini katika haya maswali? (Ayubu hafahamu habari za jua au mwezi au mizunguko ya nyota na sayari. Maarifa yake ni finyu kwa sababu umri wake wa kuishi ni mfupi.) F. Soma Ayubu 39:26-28. Mungu anamaanisha nini katika haya maswali? (Ayubu hafahamu jinsi ya kupaa, achilia mbali kubuni jinsi ndege wanavyoweza kupaa.) G. Soma Ayubu 40:1-2. Je, Mungu anampa Ayubu usikivu? (Ndiyo! Anahitaji jibu kutoka kwa Ayubu – ikiwa ana uerevu wa kutosha wa kufanya hivyo.) IV. Majibu ya Ayubu Mahakamani A. Soma Ayubu 40:3-4. Hili ni jibu la namna gani? (Ayubu anakiri kuwa hastahili kumburuza Mungu mahakamani na anatoa madai kwamba Mungu ajielezee mwenyewe.) B. Soma Ayubu 40:5. Je, Ayubu amekiri kushindwa “kesi” dhidi ya Mungu? (Anasema kuwa “hatasema tena.” Jibu ni “ndiyo,” anakiri kuwa alikuwa amekosea.) V. Mungu Kukanusha Hoja Mahakamani A. Soma Ayubu 40:6-8. Hili ni swali tofauti kabisa. Mungu anayachukuliaje malalamiko na matakwa ya Ayubu kutaka kusikilizwa? (Kwamba anaaibisha/anafedhehesha utoaji haki wa Mungu.) 1. Angalia swali hili, “Utanitia Mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki?” Watu wangapi wanamtuhumu Mungu wakati ambapo ni dhahiri kabisa (na dhahiri hata kwako) kwamba wanawajibika kwa matatizo yao wenyewe? 2. Hebu subiri kidogo! Ikiwa Ayubu ni mwenye haki (na kwa hakika ana haki), ni kwa jinsi gani jibu la Mungu ni sahihi? Vipi kuhusu Kumbukumbu la Torati 28 inayosema kuwa tabia ina matokeo yake? B. Soma Ayubu 40:15-19. Mnyama gani anayeelezewa hapa? (Inaonekana maelezo haya yanamhusu dinosau [pia dinosaria] - mnyama mkubwa sana wa zamani (mwenye umbo la kenge).) 1. Mungu anazungumzia habari gani juu ya dinosau? (Alimuumba na anaweza kumwua.) a. Je, hitimisho ni kwamba kwa kuwa Mungu alimuumba Ayubu, basi pia anaweza kumwua? C. Tutaruka mafungu yaliyosalia katika hii sura pamoja na sura inayofuata, kwa sababu zinaelezea mfululizo wa kauli zinazofanana zinazoonesha uwezo mkuu wa Mungu juu ya uumbaji. VI. Ayubu Asalimu Amri A. Soma Ayubu 42:1-3. Ayubu anakiri nini kuhusu kiwango cha uelewa wa Mungu na uumbaji wake? (Yeye ni mjinga. Haelewi chochote.) B. Soma Ayubu 42:4-6. Ayubu aliorodhesha matendo yake yote ya haki. Anatubu kutokana na nini? Kwa nini anajichukia? (Ayubu hakumtumaini Mungu wakati alipokuwa hana uelewa mkamilifu.) 1. Je, hicho ndicho wengi wetu tunapaswa kukiangalia, ikiwa tunamtumaini Mungu? C. Tunapojifunza kitabu cha Ayubu, tutaona kwamba kuna maelezo ya wazi kabisa juu ya sababu za Ayubu kuteseka sana. Kamwe Mungu hampi Ayubu hayo maelezo. Badala yake, Mungu anasema tu kile ambacho tumekipitia hivi punde. Kwa nini? Kwa nini asimwambie Ayubu kilichokuwa kinaendelea? (Tunachokiona ni kwamba Mungu alimwambia Ayubu, “Mimi ni Mungu na wewe si Mungu. Kaa chini, nyamaza kimya na unitumaini Mimi. Nina maarifa, uelewa na uwezo kamili. Kazi yako ni kunitumaini Mimi.) 1. Je, jibu hilo linakuridhisha matatizo yanapokujia? D. Soma Ayubu 42:10-16. Maisha ya Ayubu yanaishaje? (Yeye ni tajiri, amebarikiwa, ana familia mpya nzuri, na aliishi hadi kuwaona wana wa wanawe hata vizazi vinne. Alifariki kutokana na uzee.) E. Kama tutakavyoona juma lijalo, Mungu anaondoa pazia ili kutuonesha sababu hasa ya Ayubu kuteseka. Kwa nini Mungu anatuambia, lakini hakumwelezea Ayubu? (Mungu anatutaka, kama ilivyokuwa kwa Ayubu, kumtumaini tu Yeye matatizo yanapokuja. Lakini, Mungu yuko radhi kutuonesha kuwa maamuzi yake yana mantiki.) F. Rafiki, je, utamtumaini Mungu? VII. Juma lijalo: Pambano Kuu. Asante kwa kutembelea Blog yetu washirikishe na wenzako, Pia tunaomba maoni yako hapa au tupigie kwa (+255) 0769436440 Karibu Tena

Flower
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

About IVST TANZANIA

Hi my name is Gasto Alex Didas
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

MBUNGE MABULA AKAGUA SHULE NNE MPYA ZA MSINGI, ZENYE THAMANI YA TSH 1.174 BIL, ASHAURI HALMASHARI KUTUMIA MCHORO MPYA WA TAMISEMI KUOKOA MADARASA 3 KILA SHULE

Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo La Nyamagana amefanya ziara ya kikazi katika Kata nne za halmashauri ...

Popular Articles