Mkuu wa polisi Uganda atakiwa kizimbani
Mkuu wa jeshi la polisi la Uganda, Jenerali Kale Kayihura anatarajiwa kufika kizimbani leo kujibu mashtaka ya kuwatesa na kuwanyanyasa wafuasi wa upinzani.
Mashataka haya yana uhusiano na kile kinachoitwa unyama wa polisi kufuatia askari polisi kuwatandika wafuasi wa Dkt Kiiza Besigye waliokuwa wakiandamana naye kuitia barabara za mjini Kampala hadi makao makuu ya chama cha upinzani cha FDC.
Hata hivyo kuna wasiwasi wa huenda mkuu huyo asifike mahakamani.
Mwandishi wetu wa Kampala Siraj Kalyango anasema hatua ya mkuu wa polisi ya Uganda kuitwa mahakamani inafuata juhudi za mawakili wa kampuni ya uwakili ya Namugali na Walyemera kupeleka kesi mahakamani kwa niaba ya wateja wao kadha.
Wamemshtaki kinara wa polisi na pia maafisa wengine saba wa jeshi la polisi kwa ujumla kwa kuwanyanyasa wananchi.
Hata hivyo kuna shaka kuwa huenda Kayihura asifike mahakamani kutokana na matukio kadhaa.
Naibu msemaji wa polisi Namaye amenukuliwa na vyombo vya habari nchini akisema kuwa Jenerali Kayihura hatafika mahakamani kwa sababu hajapata waraka wa kumuita mahakamani.
Makao makuu ya polisi
Lakini wakili Daniel Walyemera Masumba anaeongoza kesi hiyo amekanusha hayo.
"Nakuhakikisha kuwa jenerali Kale Kaihura alipokea agizo la kumtaka afike kortini.Yeye mwenyewe ni wakili na anajua fika sheria inasema nini na jinsi tunatoa agizo hilo," ameambia BBC.
"Nikishindwa kumpa barua ya agizo nyumbani kwake naweza kufanya hivyo ofisini kwake jambo tulilolifanya. Tulimpa stakabadhi hiyo katika makao makuu ya polisi Naguru. Tuna ushahidi."
Mawakili wanasisitiza kuwa wanataka mkuu wa polisi ajitokeze mwenyewe na wala sio mjumbe wake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment