Biden atokwa na machozi akipewa medali na Obama
Rais wa Marekani Barack Obama amemtunuku makamu wake Joe Biden Medali ya Rais ya Uhuru, ambayo ndiyo nishani ya hadhi ya juu zaidi anayoweza kupewa raia nchini Marekani.
Biden, ambaye alionekana kushangazwa na hatua hiyo, alitokwa na machozi alipokuwa anatunukiwa medali hiyo.
Bw Obama amemsimu makamu huyo wa rais kwa "imani yako katika Wamarekani wenzako, kwa upendo wako kwa taifa na kwa utumishi maisha yako yote."
Tuzo hiyo imetolewa kwa Bw Biden wawili hao wanapojiandaa kuondoka madarakani Donald Trump wa Republican atakapoapishwa kuwa rais mpya tarehe 20 Januari.
Bw Biden amesema anapanga kuendelea kushiriki siasa katika chama cha Democratic.
Hakutarajia
Joe Biden, aliyeonekana kutekwa sana na hisia, alisimama na kuonekana kushangaa Bw Obama alipomlimbikizia sifa na kumtaja kuwa "chaguo bora zaidi, si kwangu tu, bali kwa Wamarekani".
Medali hiyo ilikuwa na hadhi ya ziada, kwa mujibu wa gazeti la New York Times.
Hadhi hiyo ya ziada, katika serikali za Marekani zilizotangulia, ilitunukiwa watu wachache sana, akiwemo Papa John Paul II.
Bw Obama alifanya mzaha kwamba mtandao sasa utakuwa na fursa ya mwisho ya kucheka na kufanyia mzaha kile ambacho kimekuwa kikiitwa "bromance", maana yake upendo na urafiki wa dhati kati ya Obama na Biden.
Kwenye Twitter, watu tayari wameanza kutoa maoni yao.
Wengine wanasema wanaume hao wawili ni mfano bora wa kuigwa katika uhusiano wowote ule.
Bw Biden alisema yeye ni "sehemu ya safari ya binadamu wa kipekee aliyetenda mambo ya kipekee".
Alisema kamwe hakutarajia kwamba angetunukiwa medali hiyo.
"Sikutarajia kamwe. Nilidhani tulikuwa twaja kwa Michelle kwa ajili yako, Jill na Barack na mimi na watu wengine kadha kufurahia pamoja na kusherehekea safari ambayo tumekuwa nayo pamoja.
"Bw Rais, umegonga ndipo uliposema kwamba nimemtegemea sana Jill lakini nimekutegemea sana, na nimewategemea watu wengine wengi katika chumba hiki.
Medali ya Rais ya Uhuru Marekani
- Ndiyo medali ya hadhi ya juu zaidi anayopewa raia Marekani
- Ilianzishwa mwaka 1963 na Rais John F Kennedy, ambapo iliizidi Medali ya kawaida ya Uhuru Medal of Freedom
- Wengi wa waliotunukiwa wamekuwa katika: siasa; biashara; jeshi; muziki; filamu; uanahabari
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment