Senegal waandamana kupinga ukatili
- Saa 5 zilizopita
Nchini Senegal, watu kadhaa wameandamana mjini Dakar kumuunga mkono mwanamke mmoja raia wa nchi hiyo aliyekamatwa majuma machache yaliyopita na kushtakiwa kwa makosa ya kumuua mke wa mwajiri wake huko Saudi Arabia.
Familia ya Mbayang Diop na wanaharakati wa haki za binaadam wanahofu huenda akanyongwa kwa mujibu wa sheria za Saudi Arabia.
Ripoti ya kukamatwa kwa Mbayang Diop zilikuwa tayari kwenye vyombo vya habari vya Senegal siku chache zilizopita.lakini sasa wanaharakati wa masuala ya haki za binaadam wameanzisha kampeni kwenye mitandao ya kijamii wakisihi kumuokoa Mbayang, kampeni ambayo imekuwepo kwa kipindi cha saa 24 zilizopita, kabla ya mkutano wa jumatatu uliofanyika kwenye msikiti mmoja wa katikati mwa mji wa Dakar.
Wanasiasa wanawake, wakiwemo wale wanaotoka chama tawala na upinzani, pia wafuasi wa asasi za kiraia na chama cha wafanyakazi wa majumbani walikutana kwa ajili ya kesi ya binti wa miaka 22 , ambaye aliondoka Senegal baada ya kuahidiwa kuwa atapata kazi nzuri inayolipa vizuri nchini Saudi Arabia.Badala yake, kwa mujibu wa kaka yake, binti huyo alikuwa akinyanyaswa, hivyo alimuua mke wa mwajiri wake baada ya kulumbana.
Mamlaka ya mambo ya nje ya Senegal imesema wanafuatilia kesi hiyo kwa karibu na kutangaza kuwa Balozi wa Senegal nchini Saudi Arabia atakutana na Mbayang siku ya jumatano gerezani anakoshikiliwa.
Wanaharakati wameomba huruma ya Serikali ya Senegal ili iweze kuzungumza na mamlaka za Saudi Arabia ili binti huyo arudishwe nchini mwake na kushtakiwa.
Hata hivyo mamlaka hazijasema hatua gani zitachukua.
Wanaharakati wa haki za binaadam, waliripoti visa vya unyanyasaji wanavyofanyiwa wafanya kazi wa ndani kutoka nchini Senegal walioko Saudi Arabia,Lebanon,Morocco na Algeria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment