Muhtasari: Habari kuu leo Alhamisi
- 11 Agosti 2016
Miongoni mwa habari kuu leo, watu wanne wameuawa kwa gesi ya sumu Syria, makao makuu ya IS nchini Libya yakatekwa na Clinton amemtuhumu Trump kwa uchochezi.
1. Watu wanne wauawa kwa gesi ya sumu Syria
Maafisa wa matibabu katika mji wa Syria wa Aleppo wanasema kuwa takriban watu wanne wamefariki huku wengine wengi wakijeruhiwa, katika shambulio linaloshukiwa kuwa la gesi ya sumu katika eneo linalodhibitiwa na waasi.
Gesi hiyo inadaiwa kuwa ile ya klorini.
Shambulio hilo linajiri saa chache kabla ya wanajeshi wa Urusi kusitisha vita kwa muda ili kuruhusu msaada wa kibinaadamu.
2. Serikali yateka makao makuu ya IS Libya
Vikosi vinavyounga mkono serikali nchini Libya vinasema kuwa vimeyateka makao makuu ya wapiganaji wa kundi la Islamic State katika mji wa Sirte.
Vikosi hivyo vinavyoungwa mkono na wapiganaji kutoka eneo jirani la mji wa Misrata vinasema kuwa vinadhibiti kituo cha Ouagadougou pamoja na hospitali kuu.
3. Ukraine: Putin anatafuta sababu kushambulia
Ukraine imemshtumu rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kutafuta sababu ya kulishambulia taifa hilo baada ya kudai kwamba Kiev imechagua kufanya ugaidi badala ya amani.
Hatua hiyo inajiri kufuatia madai ya idara ya usalama nchini Urusi kwamba ilitibua jaribio la vikosi maalum vya Ukraine kuhujumu miundo msingi katika eneo linalozozaniwa la Crimea.
4. Marseille hatarini kutokana na moto
Misururu kadhaa ya moto kusini mwa Ufaransa inatishia mji wa pili kwa ukubwa, Marseille.
Takriban wazima moto 1,800 wanakabiliana na moto huo wakijaribu kutengeneza ukuta ili kuilinda bandari hiyo pamoja na mji wa viungani wa Vitroles.
5. Clinton asema Trump anachochea ghasia
Mgombea wa urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amemshtumu mpinzani wake wa Republican Donald Trump kwa kuchochea ghasia, kufuatia tamko lake la haki za umiliki wa bunduki.
Bw Trump amewataka wafuasi wake wanaomiliki bunduki kumzuia Bi Clinton kufutilia mbali haki zao za kikatiba.
6. Misri yashinda medali ya kwanza Rio
Na kijana mmoja wa Misri, Sara Ahmed amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka taifa hilo kushinda medali katika michezo ya Olimpiki.
Alimaliza wa tatu katika kitengo cha kilo 69 cha ubebaji uzani, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanamke mwarabu kufikia hatua hiyo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
No comments:
Post a Comment