Tafakari Zaidi:
“Katika enzi aliyoangaziwa na sayansi na kufikiri kwa namna ambayo ilikuwa haijawahi kutokea, ‘habari njema’ ya Ukristo imekuwa ni nadharia ya kufikirika ambayo imezidi kupoteza ushawishi siku kwa siku katika utashi wa mtu, unazidi kuwa msingi usioweza kuaminika katika ujenzi wa maisha, na unazidi kuonekana si wa lazima kisaikolojia. Kule kutokuyamkinika kwa mfululizo mzima wa matukio, ulikuwa unazidi kuwa dhahiri—kwamba Mungu wa milele asiye na ukomo angeweza ghafla kuwa mwanadamu fulani katika wakati na mahali mahususi katika historia, halafu akaishia kuuawa kwa fedheha.” Kwamba maisha mafupi ya mtu mmoja, yaliyotokea kiasi cha milenia mbili kabla katika taifa la kale lisilojulikana, katika sayari inayojulikana kwa sasa kuwa kipande kidogo sana cha maada ukilinganisha na sayari zingine, inayozungukia nyota moja miongoni mwa mabilioni ya nyota katika Ulimwengu usio na hisia wenye ukubwa usiowazika—kwamba tukio lisiloweza kupambanuliwa kama hilo lingekuwa na maana yo yote kubwa na ya milele isingeweza kuendelea kuwa imani ya kuvutia kwa watu wenye akili. Ilikuwa wazi kwamba ulimwengu wote usingeweza kujishughulisha na sehemu hii ndogo sana katika ukubwa wake. Katika wimbi la matakwa ya kisasa ya matamko yote ya imani kuungwa mkono na wengi, watawala na uthibitisho wa kisayansi, umuhimu wa ukristo ulififia..”—Richard Tarnas, Passion of the Western Mind (New York: Ballantine Books, 1991), p. 305. Dhana hii ina matatizo gani? Mwandishi anakosea wapi? Nukuu hii inatufundisha nini juu ya ufinyu wa kile ambacho “sayansi na akili” vinaweza kujua kuhusu kuwapo kwa Mungu na upendo wake kwetu? Jambo hili linatuonesha nini juu ya hitaji la ukweli uliofunuliwa, ukweli ambao “sayansi na akili” ya wanadamu haiwezi kuufikia yenyewe?
Maswali ya Kujadili:
1.Wewe kama Mkristo, ungejibuje swali hili, “Mtu ni kitu gani?” Jibu lako litakuwa na tofauti gani na jibu la watu ambao hawamwamini Mungu wa kwenye Biblia?
2.Cormac McCarthy aliandika “Jinsi wafu wasivyoweza kupatwa na mauti. Mauti ni jambo ambalo walio hai hutembea nalo.” Kwa nini uelewa wetu juu ya kinachotokea baada ya kifo unatakiwa kutupatia faraja juu ya wapendwa wetu waliokufa? Je, haitupasi kupata faraja, japo kidogo, kwa kujua kwamba wapo katika amani, wamepumzika, wametengwa na mahangaiko mengi na matatizo ya maisha?
3.Unafikiri ni kwa nini hata maisha yawe mabaya kiasi gani watu wengi hutamani kuendelea kuishi, bila kujali ugumu wa hayo maisha?
4.Jadili kile tunachofundishwa na msalaba kuhusu thamani ya uhai wa mwanadamu, kuhusu thamani ya uhai wa hata mwanadamu mmoja.

No comments:
Post a Comment